Ukweli wa Mambo: Katiba Mpya – Tuangazie Mifumo Wenyewe Hasa
KATIBA MPYA ITAKUJA BALI TUANGAZIE MFUMO WENYEWE HASAMakala ya Nguvu ya Hoja kwa KSB Jumapili Januari, 2010
na Ndugu Mwandawiro Mghanga
Ninakariri, ukombozi wa wengi utapatikana wakati tutakapotoka kwa ndoto na kurudi katika dunia halisi ya harakati za kitabaka na kujizatiti ipasavyo. Ndiyo, mwaka huu tutapata katiba mpya. Wacha ije. Lakini maisha mapya nchini bado yako mbali. Maana katiba mpya ndani ya mfumo wa ubepari haijaweza wala haitaweza kuleta maisha mapya kwa wengi. Katiba ya kibepari ilitimiza jukumu lake la kihistoria wakati ilipotumiwa kuondoa mfumo wa ukabaila na kuleta ule wa ubepari. Kutoka wakati huo katiba ya kibepari inalinda mfumo wa kibepari. Nimeisoma kwa makini ruwaza ya katiba mpya ya Kamati ya Nzamba Kitonga, ikisomwa kijuujuu inaonekana kuwa ya watu wote wa Kenya. Lakini ikichambuliwa kwa undani kutoka kwa msimamo wa kitabaka itadhihirika kuwa ya kulinda ubwanyenye kwa kupoza harakati za kitabaka. Wacha ije tuendendelee kujifunza na kukua.
Kote ulimwenguni, Kenya ikiwepo, dola la ubepari pamoja na katiba zake linaongozwa na mabepari, itikadi za kibepari na adili za kibepari. Ni la kulinda mfumo wa ubepari. Nao mfumo wa ubepari ni wa kitabaka, wa unyonyaji wa mtu kwa mtu, wa mwenye nguvu mpishe mnyonge msonge. Mfumo wa vyama vingi, uchaguzi na utawala wa kidemokrasi ndani ya mfumo wa ubepari ni halali bora tu usilenge kuondoa mfumo wa ubepari. Dola za kibepari hutumiwa kuwanyonya na kuwanyanyasa wafanyikazi, wakulima makabwela na wale wote wasiyo na umilikaji wa viwanda, biashara kuu, mashamba makubwa na njia kuu za uzalishaji.
Ni la kuwatawala na kuwagandamiza wale wanaoishi kwa kutegemea ujira, wavujajasho, wakodeshaji nyumba, wale ambao ni mafukara ama walalahoi. Kwa ujanja wake, ambao ni pamoja na kujificha ndani ya katiba na demokrasi ya kibepari, dola la kibepari linaonekana kana kwamba liko kwa ajili ya taifa na kila raia pasina mapendeleo. Bali haijawezakana wala haitawezekana kuwa na usawa kati ya tajiri na maskini. Usawa huo unawezekana tu katika maandishi ya katiba wala siyo katika hali halisi ya maisha.
Kama kawaida ya katiba zote za kibepari, ruwaza ya katiba ya Kitonga imejaa orodha ya haki za binadamu, kama usawa katika sheria, uhuru wa kusema na kusambaza maoni, uhuru wa kutembea na kujumuika, haki ya matibabu, haki ya kujipatia riziki, haki ya kuwa na nyumba bora, haki ya elimu kwa kila raia, haki ya kuchagua au kuchaguliwa kiongozi, haki za wafanyikazi, haki za watoto, haki za wanawake, haki za walemavu na haki za wazee. Sawa, lakini wakati huohuo ruwaza ya katiba inalinda mali ya binafsi ambayo ni msingi wa ubepari. Inaahidi haki na usawa kwa raia wote ndani ya mfumo wa kitabaka, jambo la kuwavisha vilemba vya ukoka wengi ambao ni mafukara na wanaolilia ukombozi.
Msingi wa katiba za kibepari ni kulinda na kuabudu haki ya mtaji na mali ya binafsi. Kwa mfano, mabepari wana haki ya kuwa na mali ya binafsi na kuikuza kwa vyovyote vile hata kwa kuwanyonya na kuwanyanyasa wafanyikazi katika viwanda, makarakana, makampuni, na popote pale penye mitaji yao. Nao mafukara eti wanahakikishiwa na katiba haki ya kuwa mabepari wakitaka. Lakini, utake usitake bila mtaji huwezi kuwa bepari. Huwezi kutoka kwa tabaka la wafanyikazi na kuingia tabaka la mabepari ghafla bin vu ati kwa kuwa tu umeamua kufanya hivyo au kwa sababu unaruhusiwa na katiba. Ukweli ni kuwa uwezo wa mtu kutoka tabaka la mafukara kuingia tabaka la mabepari ni sawa na ule wa ngamia kupitia tundu la sindano.
Tukiangazia Kenya tunaona kuwa jamaa za matajiri, zenye kudhibiti uchumi wa pesa, ardhi, biashara na mali tilatila, ni zilezile tu za kutoka kale na zamani. Aidha, pengo kati ya matajiri na maskini linazidi kupanuka nchini kila siku. Chimbuko cha umaskini si kuwa maskini hawafanyi kazi kwa bidii bali ni mfumo unaohakikisha kuwa kazi na bidii ya maskini inamfaidi tajiri badala ya yeye mwenyewe. Asili ya utajiri wa tajiri si kazi na bidii ya tajiri bali ni umilikaji wa njia ya uzalishaji inayomwezesha kuwanyonya wafanyikazi. Kujigamba kuwa umepanda kutoka biashara ya makaa na kuwa bilionea wa pesa, biashara, ardhi, majumba na mali tilatila leo kutokana na bidii zako binafsi, ni kutupigia hekaya za Abunwasi.
Ruwaza ya katiba mpya imewapa wananchi wote haki za matibabu. Lakini kadiri ambapo Kenya itandelea kuwa ya ubepari, matajiri ndiyo watakaondelea kutekeleza haki hii mara nyingi zaidi kuwaliko makabwela na mafukara. Nchini leo, udaktari, mahosipitali na matibabu ni biashara kama biashara yoyote ile inayowatajirisha watu binafsi kwa kuwanyonya wagonjwa. Bila pesa ni muhali kupata matibabu yoyote, sembuse matibabu bora. Adili za udaktari, ambazo ni pamoja na kujitahidi wakati wote kuokoa maisha, hazitekelezwi katika mfumo unaoongozwa na adili ya kuchuma mali kwa vyovyote vile. Wala hakuna huruma, pesa zimekuwa na thamani kuliko maisha Kenya. Udaktari kama utaalamu wowote ule unatumiwa kuendeleza mfumo wa unyonyaji wa mtu kwa mtu.
Elimu pia imekuwa bidhaa kama bidhaa yoyote ile. Wenye hela ndiyo wenye uwezo wa kuwanunulia watoto wao elimu bora zaidi katika shule za binafsi nchini na ughaibuni. Elimu Kenya inatumiwa maksuudi kuzidisha na kuhifadhi utabaka na pengo kati ya matajiri na maskini. Na serikali haina haya wala aibu kuendeleza mfumo wa elimu unaowabagua, kuwakebehi na kuwanyanyasa watoto wa makabwela. Maana ni serikali ya mabepari.
Ndiyo, katiba mpaya ije. Bali tutumie muda wetu zaidi kuangazia mfumo wa kujamii – kiuchumi maana tusipoubadilisha na kuleta mpya na wa hali ya juu zaidi punde tutagundua kuwa katiba mpya vilevile ni mbio za sakafuni.
No comments:
Post a Comment